Na Betty Luke
Hali ya taharuki imeibuka katika bunge la Kaunti ya Isiolo kufuatia barua iliyowasilishwa kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na baadhi ya madiwani ikitaka shirika hilo kumchunguza Spika Mohamed Roba Qoto na karani Salad Boru kuhusiana na madai ya utumizi mbaya wa mamlaka na ufisadi.
Kurasa tatu za kwanza za barua hiyo yenye kurasa tano iliowasilishwa katika ofisi za EACC za Mashariki ya Juu zilizoko mjini Isiolo siku ya Jumatano ziliwashutumu wawili hao kwa tuhuma mbalimbali huku kurasa mbili za mwisho zikiwa ni mawasiliano ya Bunge ya Januari 25 ambayo yalikuwa yameelekezwa kwa Spika kutaka kuondolewa kwa Bw Boru.
Kurasa hizo mbili ni ikiwemo orodha yenye majina 17 ya madiwani, nambari za vitambulisho vyao na saini zao ikiwa na muhuri ulioonyesha ilipokelewa na Spika mnamo Januari 26 mwaka huu.
Katika barua hiyo, madiwani walieleza kutoridhishwa na Bw Boru kwa kubadilisha ruzuku ya magari ya Sh13.2 milioni kwa wenzao sita wa Chama cha UDM na kupea zabuni za Bunge kwa kampuni zinazohusishwa naye.
“…Hafai kusimamia uhasibu kwa sababu ya vitendo vya uhalifu vilivyotajwa hapo juu na ukiukaji wa Katiba,” barua hiyo ilisema.
Na ingawa aya ya mwisho ya barua hiyo yenye kurasa tatu iliyotumwa kwa EACC na iliyotayarishwa Februari 5 ilionyesha kuwa madiwani waliahidi kutuma mashahidi na kutoa ushahidi kuhusiana na madai hayo, haikutiwa sahihi licha ya kusema kuwa “Iliyoambatishwa ni saini zetu”.
Katika hali ya kushangaza, madiwani wawili kati ya watatu waliowasilisha barua hiyo katika afisi ya EACC walikuwa kati ya kumi na moja ambayo wamepinga barua hiyo na kukiri kuwa walitoa saini zao kwa barua ya kutimuliwa kwa karani pekee.
Madiwani waliowasilisha barua ya malalamiko kwa EACC ni Salesio Kiambi (Wabera), David Waithaka (Bulapesa) na Abdinoor Dima Jillo wa wadi ya Kinna.
Wabunge hao kumi na moja waliwasilisha barua kwa EACC wakisema malalamiko hayo ya awali hayakutoka kwao na kwamba ukurasa uliotiwa saini ambao ulitolewa katika mawasiliano ya Bunge ya hapo awali.
Wakiomba hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya waliowasilisha malalamiko hayo, Naibu Spika David Lemantile alikiri kuwepo kwa “tofauti” katika Bunge hilo na kusikitika kuwa yalitolewa hadharani huku akisema kuwa yangeweza kutatuliwa ndani ya Bunge.
“Tuna mizozo kati yetu ambayo tunaweza kutatua sisi kwa sisi. Wazo la kupeleka suala hilo kwa EACC halikukubaliwa kwa kauli moja. Barua ya malalamishi haina muhuri kuonyesha kwamba haikutoka kwa Bunge,” Bw Lemantile alisema.
Kuhusiana na barua hiyo ya kumtimua karani wa bunge, madiwani hao walidai, Spika Qoto aliitwa Bungeni kujibu.
Diwani wa Ngaremara Peter Losu ambaye ni mwanachama wa Bodi ya Uajiri ya Bunge la Kaunti hiyo alidai kuwa baadhi ya masuala waliyoibuliwa katika barua ya Disemba iliyopita yalishughulikiwa lakini hakutoa uthibitisho.
“Bodi iliahidi kulipa ruzuku ya gari kwa wenzetu sita baada ya pesa kupatikana,” Bw Losu alisema, akishikilia kuwa Bunge hilo halikuwa na matatizo na Spika.
Hata hivyo, madiwani hao hawakueleza ni kwa nini ni ruzuku za magari za wenzao sita kati ya 18 zilizuiliwa huku barua ya malalamishi ikidai kuwa pesa hizo zilielekezwa kwingine.
Madiwani Kiambi na Waithaka walijipata pabaya kuhusiana na mabadiliko ya ghafla huku mwakilishi wa Bulapesa akisisitiza Bw Jillo alimwomba tu ampeleke katika ofisi za EACC, bila kujua yaliyokuwa katika barua ambayo angewasilisha baadaye.
“Nilikuwa miongoni mwa walioenda EACC lakini nilifahamu yaliyokuwa katika barua hiyo katika afisi ya DCI ambapo nilimwambia Bw Jillo singeweza kuwa mshiriki wake,” Bw Waithaka alisema.






